Job 18

Bildadi Anasema: Mungu Huwaadhibu Waovu

1 aBildadi Mshuhi akajibu:
2 b“Je, ni lini utafika mwisho wa maneno haya?
Uwe mwenye busara, nasi ndipo tutakapoweza kuongea.

3 cKwa nini sisi tunafikiriwa kama wanyama,
na kuonekana wajinga machoni pako?

4 dWewe unayejirarua mwenyewe vipande vipande
katika hasira yako,
je, dunia iachwe kwa ajili yako wewe?
Au ni lazima miamba iondolewe mahali pake?


5 e“Taa ya mwovu imezimwa,
nao mwali wa moto wake umezimika.

6 fMwanga hemani mwake umekuwa giza;
taa iliyo karibu naye imezimika.

7 gNguvu za hatua zake zimedhoofishwa;
shauri lake baya litamwangusha.

8 hMiguu yake imemsukumia kwenye wavu,
naye anatangatanga kwenye matundu ya wavu.

9 iTanzi litamkamata kwenye kisigino;
mtego utamshikilia kwa nguvu.

10 jKitanzi kimefichwa ardhini kwa ajili yake;
mtego uko kwenye njia yake.

11 kVitisho vimemtia hofu kila upande,
na adui zake humwandama kila hatua.

12 lJanga linamwonea shauku;
maafa yako tayari kwa ajili yake aangukapo.

13 mNayo yatakula sehemu ya ngozi yake;
mzaliwa wa kwanza wa mauti atakula maungo yake.

14 nAtang’olewa kutoka usalama wa hema lake,
na kupelekwa kwa mfalme wa vitisho.

15 oMoto utakaa katika hema lake;
moto wa kiberiti utamwagwa juu ya makao yake.

16 pMizizi yake chini itakauka
na matawi yake juu yatanyauka.

17 qKumbukumbu lake litatoweka katika dunia,
wala hatakuwa na jina katika nchi.

18 rAmeondolewa nuruni na kusukumiwa gizani,
naye amefukuzwa mbali atoke duniani.

19 sHana mtoto wala mzao miongoni mwa watu wake,
wala aliyenusurika mahali alipoishi.

20 tWatu wa magharibi watashangaa yaliyompata;
watu wa mashariki watapatwa na hofu.

21 uHakika ndivyo yalivyo makao ya mtu mwovu;
ndivyo palivyo mahali pake mtu asiyemjua Mungu.”
Copyright information for SwhKC